Wanamgambo wa al-Shabab hukusanya mapato makubwa kuliko serikali ya Somalia

  • Mary Harper
  • Muhariri wa Afrika BBC

Wakitumia vitisho na vurugu, kundi la wanamgambo wa Kiislamu lenye makao yake nchini Somalia al-Shabab linaongeza mapato mengi kama vile mamlaka ya nchi hiyo, ripoti inasema

Wanamgambo hao hukusanya karibu dola milioni 15 kwa mwezi, na zaidi ya nusu ya pesa ikitoka mji mkuu, Mogadishu, Taasisi ya Hiraal ilisema.

Biashara nyingine hulipa kundi hilo la jihadi na serikali inayotambuliwa na jumuia ya kimataifa.

Al-Shabab imekuwa ikipambana na serikali hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja.

Kundi hilo linadhibiti sehemu kubwa ya kusini mwa Somalia na kati lakini limeweza kupanua ushawishi wake katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali iliyoko Mogadishu.

Ripoti hiyo inaelezea kama njia "ya kikatili" jinsi kikundi kinavyochukua pesa kutoka kwa watu wa vijijini.

"Hofu na tishio la maisha yao ndio motisha pekee inayowasukuma walipa ushuru wa al-Shabab," ripoti inasema.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Hiraal, tofauti na serikali ya Somalia, al-Shabab "inaendesha ziada kubwa ya kifedha" kwani kiwango cha pesa inachokusanya kinaongezeka kila mwaka, wakati gharama zake za utendaji zinabaki kuwa sawa.

Kampuni zote kuu nchini Somalia huwapa wanajihadi hao pesa, kwa njia ya malipo ya kila mwezi na "zakat" ya mwaka (sadaka ya lazima) ya asilimia 2.5 ya faida ya kila mwaka, inasema ripoti hiyo, ambayo inategemea mahojiano na wafuasi wa al-Shabab, Wasomali wafanyabiashara, maafisa wa serikali na wengine.

Wafanyabiashara katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali wanalalamika lazima walipe fedha kwa wanamgambo na serikali.

Hizi ni pamoja na zile zilizo katika kitongoji vya miji karibu na Mogadishu, ambako serikali ipo, na zile zilizo katika miji ya Bossasso na Jowhar, na kwa kiwango kidogo Kismayo na Baidoa, ambazo zote ziko nje ya udhibiti wa wanamgambo.

Bandari ya Mogadishu ni chanzo kikuu cha mapato kwa serikali ya Somalia. Hatahivyo, bidhaa zinazoingia pia "hutozwa ushuru" na wanajihadi wanaopata meli za shehena kutoka kwa maafisa wa bandari.

Taasisi ya Hiraal inasema wafanyakazi wengi wa serikali hutoa sehemu ya mishahara yao kwa al-Shabab kwa matumaini kwamba kundi hilo litawaacha licha ya kuwa watu wanaolengwa.

Wafanyakazi wa serikali na watu wengine wanaofanya kazi katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali pia wanaelezea jinsi waasi wanavyowasiliana nao kwa simu ya rununu kudai pesa.

Kamanda wa Jeshi awalipa al-Shabab

Katika maeneo yanayodhibitiwa na al-Shabab, watoza ushuru wa kijihadi huenda moja kwa moja kwa wafanyabiashara na kudai malipo.

Kamanda katika jeshi la Somalia alielezea jinsi "alivyotuma pesa kwa al-Shabab licha ya kuwa kwenye vita na kundi hilo".

Askari huyo alielezea jinsi mtu ambaye alikuwa akimjengea nyumba aliacha kazi ya ujenzi na akaondoka baada ya kamanda kukataa kulipa ada kwa wanamgambo.

Magari yanayosafirisha vifaa vya ujenzi pia yalisimama kuja kwenye eneo la ujenzi baada ya wao pia kutakiwa kulipa.

"Mwishowe nililazimika kuchagua kuacha kazi ya ujenzi au kulipa al-Shabab," alisema kamanda.

"Cha kusikitisha, niliwalipa dola 3,600 (Pauni 2,750) na nyumba yangu ilikamilishwa," alisema.

Ripoti hiyo inasema wanamgambo huitazama kwa karibu sekta inayoongezeka ya mali isiyohamishika kama wanavyofanya kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Wakala wa mali katika mji wa bandari ya kusini wa Kismayo alielezea jinsi mwenzake alivyoitwa na wanamgambo, "akipewa maelezo ya shughuli walizofanya na kuamuru kulipa kiasi kisicho na mjadala - na kutakiwa kulipa kile haswa al-Shabab walichodai".

Ikijifanya kama serikali ndogo, al-Shabab ndio chombo pekee nchini ambacho kinakusanya mapato katika maeneo ya vijijini. Inaweka ushuru kwa mifugo, kwenye mazao, hata juu ya matumizi ya rasilimali za maji.

Kikundi cha wanamgambo kilielezea kwa namna gani, katika maeneo ambayo inadhibiti, ni wakulima tu ambao wanalipa pesa kwa umwagiliaji wanaweza kutumia mito na mifereji kumwagilia mashamba yao.

"Mkulima alilalamika kwamba alilazimishwa kulipa 'ushuru wa operesheni' kwa trekta lake hata wakati ilikuwa halifanyi kazi kutokana na hitilafu ya kiufundi."

'Malipo sio hiyari'

Wafanyabiashara wengi, wafanyakazi wa serikali na wengine ambao hulipa pesa kwa al-Shabab waliwaambia watafiti wa Hiraal wanafanya hivyo tu kwa hofu.

"Kulipa ushuru wa al-Shabab sio mradi wa hiyari."

Wale wanaokataa ama wanauawa, wanalazimishwa kufunga biashara zao au kukimbia nchi.

Wengine wanahisi inafaa wakati wao wanalipa pesa kwa al-Shabab wapate huduma kama faida. Tofauti na serikali, wanamgambo wana uwezo wa kutoa kiwango fulani cha hakikisho la usalama.

"Ushuru uliolipwa katika vituo vya ukaguzi vya al-Shabab huhakikisha kupita salama katika eneo lote la al-Shabab na katika maeneo yanayoshikiliwa na serikali ambapo wanamgambo wanafanya kazi."

Ripoti hiyo inaelezea jinsi wanamgambo wanavyotatua mizozo kati ya wafanyabiashara na kudhibiti utengenezaji wa bidhaa zingine za kuuza nje kama malimao.

Hiraal anasema njia pekee ya kuwazuia wanamgambo hao kukusanya mapato kwa njia hii ni kuboresha hali ya usalama, kwa hivyo wafanyabiashara na wengine wanaweza kufanya kazi bila kuingiliwa na al-Shabab.

Kwa kuwa kundi hilo limekuwepo kwa zaidi ya muongo mmoja na linaendelea kufanya mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali, itaonekana kuwa wanamgambo wataweza kuendelea kupata pesa, bila kujali wako wapi Somalia, kwa kipindi kijacho.