Uchaguzi Tanzania 2020; Kwanini wagombea huchukua likizo katikati ya kampeni?

  • Markus Mpangala
  • Mchambuzi, Tanzania

Mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu ni fursa ya kukuza, kufafanua ilani, sera na kuonesha uhodari wa wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani ili kutengeneza mazingira ya kuvutia wapigakura zaidi na ukamilifu wa mchakato wa demokrasia.

Ni sehemu inayompatia mgombea na chama chake fursa ya kuonesha hisia zake juu ya masuala mbalimbali kwenye maeneo wanayopita kuomba kura pamoja na kueleza watafanya nini zaidi mara baada ya kuchaguliwa kushika nyadhifa wanazoombea kura.

Mikutano hiyo ni mchakato wa uchaguzi na mahali pa kupata mrejesho kutoka kwa wananchi, wafuasi na wanachama wa chama husika ambao wapo tayari kusikiliza nini kitafanyika katika eneo lao.

Licha muda mchache wa kuhutubia wapigakura, lakini mgombea anatakiwa kutembelea zaidi ya mikoa 30 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatoa ratiba kamili za wagombea ili kufanikisha mikutano hiyo. Hata hivyo uchaguzi wa mwaka 2020 umekuwa tofauti na ule uliopita wa mwaka 2015.

Katika uchaguzi wa mwaka huu wa 2020 tumeshuhudia baadhi ya wagombea wakichelewa kuanza mikutano ya kampeni, kuchukua likizo katikati ya kampeni, kusafiri kwenda nje ya nchi wakati kampeni zimepamba moto, pamoja kuadhibiwa na Kamati ya Maadili ya Tume ya uchaguzi kwa sababu mbalimbali.

Kimsingi, swali linalotaradadi katika duru za kisiasa na kuibua hamu na ghamu ni kwanini wagombea wanachukua likizo wakati kampeni zimepamba moto?

Mathalani ratiba ya mgombea inaweza kuonesha atakuwa likizo kwa siku kadhaa kisha kuendelea na ratiba nyingine baada ya mapumziko hayo, hali ambayo ni tofauti na kampeni za mwaka 2015 ambapo takribani wagombea wote walikuwa na hekaheka za kuomba maeneo mbalimbali nchini humo.

Ukiacha adhabu ya kufungiwa mikutano ya kampeni zake na Kamati ya Maadili ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, mgombea wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema, Tundu Lissu hajawahi kuchukua mapumziko yoyote tangu kufunguliwa rasmi mikutano ya kampeni ya urais, ubunge na udiwani Agosti 26 mwaka huu, ambapo alianzia katika viwanja vya Zakheim katika jimbo la Mbagala jijini Dar es salaam.

Tundu Lissu amezunguka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara akihutubia maelfu ya wafuasi wake na wapigakura pamoja na kumuombea kura mgombea wa chama cha ACT Wazalendo upande wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad.

Mgombea wa CCM John Magufuli tangu kuanza mikutano ya kampeni amechukua likizo mara mbili. Awamu ya kwanza alichukua likizo ya siku 4 na awamu ya pili alipumzika kwa siku 7 kabla ya kuendelea na mikutano mingine. Taarifa kutoka CCM zinaonesha kuwa awamu ya tatu itakuwa Oktoba 27 mwaka huu ambapo atakuwa likizo ikiwa ni siku moja kabla ya kupiga kura Oktoba 28.

Kabla ya likizo hiyo Oktoba 26 Magufuli atasafiri kutoka Manyara kuelekea Dodoma pamoja na kufanya mikutano katika maeneo ya Kondoa, Chemba na baadaye kuwasili Nyerere Square ambako CCM wamepanga mikutano yao kampeni za urais.

Kwa upande wake mgombea wa ACT Wazalendo, Bernard Membe baada ya uzinduzi wa kampeni zake mkoani Lindi aliondoka nchini ghafla kwenda Dubai. Mjadala ukaibuka iwapo ni kukosa fedha za kampeni au uwezo mdogo wa kuzungumza na wananchi.

Katika siku hizo asizofanya kampeni ikiwemo kusafiri kwenda Dubai inaweza kutafsiriwa kuwa naye alikuwa 'likizo' ya mikutano ya kampeni. Watu wa karibu na Membe wamesema mgombea huyo alisafiri kwenda Dubai kwa nia ya kufanya uchunguzi wa afya yake pamoja na mambo mengine ya kiuchumi na diplomasia.

Je ni sababu zipi mgombea huchukua likizo?

Inaelezwa kuwa kusafiri umbali mrefu kwa kutumia vyombo vya usafiri iwe wa anga, ardhini au majini, kuhutubia mikutano mingi.

Safari za huku na huko wakati wa kutoa hotuba, kubanwa na ratiba ya mikutano ya Kampeni inayozingatia muda na mahali, ni sababu zinazochangia wagombea kuchukua likizo katikati ya kampeni za uchaguzi mkuu bila kujali hali yoyote ya kuelemewa au kuwashinda washindani wao.

Mtaalamu mmoja wa masuala ya afya nchini Tanzania amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa, "Uchovu ni sababu tosha.

Lazima wapumzike, sababu ya kusongwa na mambo mengi wakati wa kampeni kwahiyo wao kama binadamu lazima wapumzike.

Mwili huelemewa, lakini wengine umri wao unachangia kuchukua likizo maana kuongea muda mrefu si jambo dogo, nguvu zinapungua na kusababisha Uchovu.

Kwa Lissu anastahimili hayo kwa sababu ya uimara wa afya yake, anaonekana kuwa na nguvu hasa tukizingatia umri wake."

Je, nini tafsiri yake kisiasa?

Hatua yoyote anayochukua mgombea na chama chake huwagusa wapigakura,wafuasi,wanachama na washindani wake.

Hapo ndipo huibua mjadala juu ya sababu za kuchukua likizo, huku baadhi ya washindani wakiibua utani kuwa huenda mgombea wanayeshindana naye ameshindwa kuendelea na kampeni dhidi yao.

Dkt. Richard Mbunda, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala bora wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam amemwambia mwandishi wa makala haya, "Kuna sababu mbili kubwa.

Mosi, mchakato wa kampeni una misongamano mingi kiakili na kimwili. Wanatumia usafiri wa magari na anga, lakini wanachoka, wanaongea kwa sauti kubwa wanachoka zaidi.

Ndiyo maana kwenye kampeni za urais mwaka 2010 mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete alidondoka jukwaani kwa sababu ya uchovu.

Kwahiyo wanahitaji kupumzika ili kurejesha nguvu mwilini,

Ameongeza, "Sababu ya pili, ni lazima kufanya tathmini mara kwa mara juu ya mchakato wa kampeni na kubadili mbinu au kuongeza kasi katika maeneo fulani kuvutia zaidi wapigakura maeneo hayo.

Ili ufanye tathmini unahitaji kupumzisha ratiba ya kampeni, kwa malengo ya kuja na mbinu za ziada kwenye mikutano na sera,"

Alipoulizwa, kwanini mgombea wa Chadema Tundu Lissu hajachukua mapumziko katikati ya kampeni zake mbali na kusimamishwa na Kamati ya Maadili ya Tume ya taifa ya Uchaguzi, Dkt Munda alisema, "Ningekuwa mgombea wa urais kwa namna yoyote na umri huu nina uhakika ningefika kila kona ya mikoa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa sababu nina nguvu na afya ya kufanya yote hayo. Naamini Tundu Lissu ana nguvu hiyo kulingana na umri wake. Kampeni za mwaka 2015 Edwaard Lowassa hakuweza kutumia muda mwingi mikoani, badala yake akawa anatoka jijini Dar es salaam kwenda mikoani safari moja au mbili kisha anarudi tena jijini humo.

Ndivyo inavyokuwa, umri wake haukuwa sawa na washindani wake,"