Mesut Ozil: Je hii ndio sababu ya kiungo huyo kuwachwa nje ya kikosi cha Arsenal?

Ozil ameichezea Arsenal mara 254

Kiungo huyo wa kati alyewahi kushinda kombe la dunia Mesut Ozil amewachwa nje ya kikosi cha ligi ya Premia na kile cha kombe la Yuropa na kusema kwamba utiifu ni vigumu kuupata siku hizi.

Mkufunzi wa Gunners Mikel Arteta alisema kwamba amefeli kuelewana na kiungo huyo mchezeshaji wa Ujerumani na kwamba kuwachwa kwake nje ni uamuzi wa timu.

Hatahivyo baadhi ya mashabiki wa Arsenal wamesema kwamba kuwachwa kwake nje kunatokana na matamshi yake kuhusu mateso wanayopitia Waislamu wa kabila la Uighurs nchini China.

Katika taarifa yake katika mtandao wa kijamii siku ya Jumatano , Ozil mwenye umri wa miaka 32 aliandika:

''Nitaendelea kuifanya mazoezi na kutumia sauti yangu dhidi ya ukiukaji wa haki za kibinadamu ili kutetea haki''.

Je ni nini kilichosababisha matamshi hayo ya China?

kilichotokea

Mwaka 2018, uchunguzi wa BBC ulibaini kwamba takriban watu milioni moja wengi wao kutoka katika jamii ya Uighurs walio Waislamu nchini China walidaiwa kukamatwa na kuzuiwa bila kushtakiwa katika jela kubwa.

Disemba iliopita Ozil, ambaye ni Muislamu , alitoa chapisho katika mtandao wa kijamii akiwaita watu wa jamii ya Uighurs mashujaa ambao wanakataa kushtakiwahuku akiikosoa China na Waislamu walionyamaza.

Arsenal ilijiondoa kutokana na matamshi ya Ozil ikisema klabu hiyo haingilii masuala ya kisiasa.

China mara kwa mara imekataa kuwatesa watu wa jamii ya Uighurs nchini humo `na kusema kwamba wanasomeshwa katika vyuo tofauti ili kukabiliana na misimamo mikali ya kidini miongoni mwao.

Baada ya chapisho hilo , Ozil aliondolewa katika video ya pro Evolution soccer 2020 na mechi ya Arsenal dhidi ya Man City ikaondolewa katika matangazo ya moja kwa moja ya chombo cha habari cha CCTV.

Msemaji wa waziri wa masuala ya kigeni nchini China alisema kwamba Ozil amedanganywa na habari bandia hatua iliomfanya kutoa matamshi hayo.

Je ameichezea Arsenal tangu matamshi hayo ya kwanza?

Mesut Ozil

Ozil alichapisha picha hii katika mtandao wa kijamii wiki iliopita.

Ozil alikuwa amewachwa nje na mkufunzi aliyeondoka Unai Emery kabla ya kurudi katika ,kikosi hicho chini ya ukufunzi wa kaimu meneja Freddie Ljungberg mwanzo wa mwezi Disemba 2019.

Baada ya kuajiriwa kwa Arteta kuwa mkufunzi wa kudumu baadaye mwezo huo , mwezi ambao Ozil alitoa matamshi hayo, mchezaji huyo wa Ujerumani alianzishwa katika mechi 10 za ligi ya Premia kabla ya mlipuko wa corona kusababisha likizo ya miezi mitatu mnamo mwezi Machi , lakini hajaonekana akivalia tishati ya Arsenal.

Tangu alipojiunga na Arsenal kutoka Real Madrid miaka saba iliopita , Ozil amefunga magoli 44 katika mechi 254 katika madhindano yote akiichezea Arsenal.

Alisema siku ya Jumatano kwamba amekasirishwa na hatua ya kutoshirikishwa katika mechi za Premia katika msimu huu.

''Baada ya kuandikisha kandarasi mpya 2018, niliahidi kutii klabu hii, naipenda Arsenal na inanihuzunisha kwamba hilo halifikiriwi''.