Je, ushauri wa kuvunjwa kwa bunge la Kenya uliotolewa na jaji mkuu David Maraga kwa rais Kenyatta una maana gani?

  • Profesa Hezron Mogambi
  • Mhadhiri Chuo Kikuu cha Nairobi

Hivi majuzi, Jaji mkuu wa Kenya David Maraga alimshauri Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuvunja bunge.

Sababu kuu aliyoitoa Jaji Mkuu ni kushindwa kwa bunge la Kenya kupitisha sheria kuhusiana na maswala ya kijinsia hali inayopelekea wabunge wa kike kuwa wachache kuliko inavyohitajika katika katiba ya nchi.

Katika barua kwa Rais Kenyatta, Jaji Maraga alisema kwamba kushindwa kuwa na wabunge wengi wa kike ni ukiukaji wa katiba na ubaguzi dhidi ya wanawake.

Katiba inasema kwamba jinsia moja haiwezi kudhibiti zaidi ya thuluthi mbili ya viti vya bunge. Hata hivyo, wanawake wana viti vichache ikilinganishwa na viti 116 vinavyohitajika katika bunge hilo la wabunge 350.

''Bunge limefeli ama kupuuza sheria zinazohitajika kuidhinisha sheria hiyo ya jinsia, licha ya maagizo manne ya mahakama,'' alisema Jaji Maraga.

Kisheria alitarajiwa kumshauri rais kulivunja bunge, aliongezea.

Kwa sasa kuna wabunge wa kike wapatao asilimia 23 katika mabunge mawili ya Kenya (Seneti na bunge la kitaifa) — asilimia ambayo inajumuisha viti 47 ambavyo vimetengewa wanawake tu nchini Kenya katika kaunti 47 nchini Kenya.

Utata wa kikatiba

Hata hivyo, ushauri huu wa Jaji Maraga haukutoa makataa kwa Rais Kenyatta, na hali inayoweza kumruhusu Rais Kenyatta kuamua kupuuzilia mbali ushauri huo hadi wakati hatamu yake itakapomalizika mwaka wa 2022 uchaguzi mkuu wa Kenya utakapofanyika kulingana na katiba ya Kenya.

Kulingana na katiba ya Kenya 2010, nchi ilikuwa na miaka mitano kuunda na kutekeleza sheria kuhakikisha kuwa watu wa jinsia moja si zaidi ya theluthi tatu katika uteuzi wa taasisi za umma.

Kulingana na Jaji Maraga, mahakama ya upeo chini ya aliyekuwa Jaji mkuu Willy Mutunga iliagiza bunge kuidhinisha sheria hiyo kufikia tarehe 27, Agosti 2015. Jaji huyo alisema kwamba pingamizi kadhaa ziliwasilishwa mahakamani zikilitaka bunge kuidhinisha sheria hiyo.

Bunge "likishindwa kuunda sheria inayohitajika," Maraga alisema kwenye taarifa yake, "Ni jukumu langu la kikatiba kukushauri, rais wa jamhuri ya Kenya, jukumu ambalo sasa nalitekeleza, kuvunja bunge la Kenya."

Hatua ya Jaji Mkuu Davidi Maraga wa Kenya kumshauri Rais Kenyatta kuvunja bunge imeleta utata kwenye siasa za Kenya kwa sababu kadhaa.

Kwanza kabisa, wabunge ambao wanaonekana kulengwa na kuathiriwa zaidi na hatua hii ikiwa itachukuliwa na Rais Kenyatta wanapinga kabisa ushauri huo kuhusu kuvunjwa kwa bunge huku baadhi ya wanasheria wakipinga na wanaharakati wa usawa wa kijinsia wa mashirika ya kiraia wakiunga mkono kama njia ya kupambana na hali ya kutofuata sheria na katiba nchini Kenya.

Kama ilivyokuwa mnamo Septemba mwaka wa 2017 wakati Jaji David Maraga alipoiongoza mahakama ya kilele katika kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa Urais nchini Kenya, hatua hii ya sasa ya jaji Maraga imeanzisha malumbano ya kisiasa na kisheria nchini Kenya.

Kwanza, ni kuhusu utekelezwaji wa hatua na sheria yenyewe. Je, ushauri wa jaji Maraga unaweza kutekelezwa kisheria kama ilivyo na kusuluhisha suala tata la kijinsia linalokumba usawa wa kijinsia katika taasisi za umma za Kenya?

Tatizo kubwa kuhusiana na jambo hili ni kwamba hata kama sheria ingepitishwa bungeni, je, kutekelezwa kwake kungekuwaje? Kwa mfano, ikiwa rais atavunja bunge, maelekezo haya ya sheria yatatekelezwaje bila mfumo mzima wa sheria na sheria ya vyama kuhusishwa? Na iwapo wabunge wapya watakaochaguliwa watakiuka sheria na katiba ilivyo, je, bunge litavunjwa tena? Haya ni maswali muhimu sana kama mjadala unaoendelea nchini Kenya kwa sasa.

Jukumu ni la nani?

Pia, kuna utata mwingine ambao unahusiana na utekelezwaji wa katiba ya Kenya 2010. Sheria nyingi ambazo zilihitaji kupitishwa, zilipitishwa na bunge la kitaifa na wala si seneti.

Kifungu cha 261 (2) cha katiba ya Kenya kinalipa bunge la kitaifa uwezo wa kuongeza wakati unaofaa kuchukuliwa ili kupitisha na kutekeleza baadhi ya sheria. Je, seneti inafaa kuadhibiwa pia iwapo bunge la kitaifa litashindwa kuunda na kutekeleza ama kuongeza muda unaohitajika kupitisha sheria fulani inayohitajika?

Kifungu cha 259 cha katiba kama ilivyoelezwa na uamuzi wa mahakama ya kilele ya Kenya inahitaji kwamba katiba ifafanuliwe na kuelezwa kwa namna ambayo inasaidia kuitekeleza, kwa malengo yake, maadili na kanuni. Je, hali hii iliafikiwa kabla ya ushauri wa jaji Maraga kutolewa?

Na ikiwa ni hivi, ikiwa Rais Kenyatta atafuata ushauri wa jaji Maraga na kuvunjilia mbali bunge, je, kitakachofuata ni uchaguzi mkuu ama uchaguzi mdogo? Hili halijabinishwa wazi na katiba ya Kenya, 2010. Zaidi ya haya, kifungu 101 (1) cha katiba kinaeleza kwamba uchaguzi mkuu wa wabunge utafanywa mnamo Jumanne ya pili mwezi wa Agosti, kila mwaka wa tano.

Wataalam wengi wa sheria wanaeleza kwamba kuna utata kati ya yanayoelezwa kwenye kifungu cha 101(1) na 102(1) - ambacho kinaeleza kuhusu muhula wa kila bunge ambao unafaa kuwa tarehe ya Uchaguzi Mkuu unaofuata - na nguvu za kikatiba alizonazo Rais kulingana na kifungu 261(7).

Kuwachagua watu kwenye nyadhifa sita

Aidha, aina sita za uchaguzi ambazo wananchi hushiriki na kupiga kura - urais, ubunge, useneta, mwakilishi wa akina mama, mwakilishi wa wodi, na gavana - zinafaa kufanyika siku moja. Je, hii ina maana kwamba bunge likivunjwa, rais, magavana, na wawakilishi wodi pia watahitaji kushiriki katika uchaguzi mwingine?

Je, vifungu hivi vinaonyesha ukinzani kwenye katiba? Ni nini kitatokea iwapo bunge litavunjwa? Iwapo uchaguzi utafanywa, je wabunge watahudumu kwa muda uliobaki tu hadi 2022? Kwa misingi hii, ni nini maana ya "bunge jipya" kama inavyoelezwa kwenye kifungu cha 261 (8)?

Kifungu cha 100 cha katiba ya Kenya kinawapa jukumu wabunge kuunda na kutekeleza sheria zinazoendeleza uwakilishi bungeni wa wanawake, walemavu, vijana, na wale waliotengwa.

Je, sheria kama hizo zinaweza kutungwa bila kubadilisha katiba na kuongeza idadi ya wabunge kama inavyoelezwa kwenye katiba? Je, inawezekana kwamba bunge na jinsi linavyofanya kazi linaweza kubadilishwa na kufuata sheria inayohusu jinsi bila kuwa na kura ya maamuzi yenye nia ya kubadili baadhi ya vipengele?

Kifungu cha 27(3) kinaharamisha ubaguzi. Wakenya wanafaa kufurahia haki zao kwa kuwachagua wawatakao. Kila mmoja ana haki ya kufanya uchaguzi wake kwenye siasa za nchi na kushiriki katika siasa hizo.

Je, itakuwa ni kitendo cha kiubaguzi iwapo maeneo bunge fulani yatatengwa kwa minajili ya jinsi fulani mahususi? Je, mtu anaweza kulazimishwa kupiga kura kwa njia fulani ili kufikia masharti ya sheria ya kijinsia?

Ratiba ya Tano ambacho ni kiambatisho katika katiba ya Kenya hakielezi chochote kuhusu kifungu cha 27 (8) na 81 (b) ambacho kinatwika serikali kuchukua hatua za kuunda sheria na zile za kiusimamizi ili kutekeleza kanuni hiyo ya kijinsia kuwa idadi isiyozidi theluthi mbili ya jinsia moja haifai kuwepo kwenye nyadhifa na nafasi za kuteuliwa ama kuchaguliwa kwenye taasisi zetu

Suala la muda wa kutekeleza ushauri

Suala lingine kuhusiana na ushauri wa jaji mkuu Davidi Maraga ni kuhusu muda wa kutekeleza ushauri huu wa jaji muu kama inavyoelezwa kwenye katiba.

Wakosoaji wa ushauri wa jaji Maraga kwa Rais Kenyatta wanasema kwamba katiba haijatoa makataa katika kuundwa kwa sheria kama hizo na bunge la Kenya. Je, sheria inayohusu suala la kijinsia inaeleza bayana kuwa lazima itekelezwe ndani ya muda wa miaka mitano?

Kulikuwepo na majaribio yasiyopungua 10 kuhakikisha kuwa yanayoelezwa kwenye vifungu vya 27 (8), 81(b) na (c) na kifungu 100 yanatekelezwa.

Je, baada ya wabunge kuchaguliwa, wanafaa kushurutishwa kupiga kura ama kuwa na maoni ya aina fulani? Hii ni kwa sababu kuna uhuru wa maoni na wabunge hupiga kura kulingana na maoni yao binafsi nay ale ambayo yamefikishwa bungeni. Je, hali hii si njia moja ya kuonyesha kuwa idara ya mahakama inaisimamia bunge kwa kuishurutisha kufanya kazi yake kwa namna fulani ilhali kila kitengo kina uhuru wa kufanya kazi yake kulingana na katiba?

Kesi yawasilishwa mahakamani

Huku maswali mengi yakiendelea kuibuka, kesi zinaendelea kumewasilishwa mahakamani kupinga hatua ya jaji mkuu kumshauri Rais Kenyatta kuvunja bunge.

Juma lililopita, Mahakam kuu, kupitia kwa Jaji Weldon Korir ilisitisha kwa muda kuchukuliwa kwa hatua yoyote kuhusiana na swala hilo na kuagiza kwamba stakabadhi kuhusiana na kesi hiyo ziwasilishwa kwa jaji mkuu ili aunde kundi la majaji wasiopungua watatu ambao watasikiliza kesi hiyo katika kesi ambayo itatajwa tena mahakamani tarehe 7 Oktoba.

Amri hii ya mahakama inamruhus Rais Uhuru kutochukua hatua yoyote kuhusiana na ushauri wa jaji mkuu wa kuvunja bunge. Tayari, chama cha mawakili cha Kenya kilikuwa kimempa Rais hadi Oktoba 12 kuvunja bunge la sivyo kiongoze maandamo nchini Kenya.

Wakati huo huo, wabunge kupitia kwa tume ya huduma za bunge wamewasilisha kesi katika mahakama kuu ya Kenya wakidai kuwa ushauri huo wa jaji mkuu kuvunja bunge la Kenya na kusababisha uchaguzi wa wabunge kinyume cha katiba ya Kenya kuhusiana na kifungu 131(2) pamoja na kifungu 261(7) cha katiba ya Kenya. Pia, wabunge wamedia kwamba ushauri huo wa kuvunja bunge unakwenda kinyume cha katiba inayowapa uwezo Wakenya, uwezo ambao unatekelezwa kupitia kwa bunge.

Chama cha Thirdway Alliance pia kimewasilisha kesi mahakamani kuhusiana na swala hili na huenda kesi nyingine zikawasilishwa kuunga ama kupinga hatua ya kuvunja bunge la Kenya.

Yamkini, vita vya kikatiba mahakamani kuhusiana na ushauri wa jaji mkuu kwa Rais Kenyatta kuvunja bunge ndilo tukio kuu linalofuata. Haya huenda yakaendelea hivyo hadi mahakama ya kilele ambako jaji mkuu ndiye rais na ndiye aliyetoa ushauri huo.

Kwa jumla, kinachosikitisha ni kwamba ingawa wabunge walikuwa na miaka tisa na nusu kuratibu na kupitisha kanuni zinazohitajika kufikia matarajio ya katiba kuhusiana na jinsia pamoja na kupuuza uamuzi wa mwaka wa 2015 wa jaji Joseph Onguto, mambo huenda yakawapata wabunge wa Kenya pabaya na nchi kwa jumla.

Iwapo mwishowe bunge litavunjwa na Rais Kenyatta, basi tume ya uchaguzi itawajibika kuandaa uchaguzi na kueleza ni lini uchaguzi wa wabunge katika maeneo yote ya bunge utafanyika.