Virusi vya corona: Dawa ya dexamethasone ni nini na inafanya kazi vipi?

Dexamethasone in tablet form

Dawa ya dexamethasone inatumiwa mtu akiwa anafura mwili na kwa hali mbalimbali mfano kwa walio na saratani au ugonjwa wa yabisi kavu imepongezwa na wengi kama yenye kuleta matumaini kwa wagonjwa mahututi wa virusi vya corona.

Majaribio yaliofanywa Uingereza yamethibitisha kwamba inaweza kuokoa maisha ya watu - ikiwa ya kwanza kabisa kutoa matokeo ya aina hiyo na pia imeidhinishwa kuanza kutumiwa mara moja na hospitali za Uingereza.

Hii ni dawa gani?

Dexamethasone ni dawa ya steroidi yaani yenye kubadlisha homoni - ambayo inapunguza uvimbe wa mwili kulingana na homoni inayotengenezwa ndani ya mwili.

Dawa hii inafanya kazi vipi?

Dawa hii inafanyakazi kwa kupunguza kinga ya mwili.

Maambukizi ya virusi vya corona husababisha mwili kufura wakati unajaribu kukabiliana na ugonjwa huo.

Lakini wakati mwengine mfumo wa kinga ya mwili hutikisika kupita kiasi na hali kama hizi ndio zinaweza kusababisha vifo - hali inayotakiwa kutokea wakati mwili unashambulia maambukizi huishia kuvamia seli za mwili wenyewe.

Dexamethasone inatuliza hali hii.

Kwahiyo dawa hii inakuwa yenye ufanisi kwa watu ambao wako hospitali tayari na wanapumua kwa usaidizi wa oksijeni, au mashine za kupumua - wale ambao ni mahututi.

Dawa hii haifanyi kazi kwa walio na dalili za wastani na kukandamiza mfumo wa kinga wakati huu hakutakuwa na maana.

Je ufanisi wake ukoje?

Kulingana na wanasayansi ambao wanafanya majaribu hayo, kifo kimoja kati ya watu watatu kunaweza kuzuiliwa miongoni mwa wagonjwa mahututi.

Kwa wagonjwa wanaotumia oksijeni, inaweza kuzuia kifo cha mtu mmoja kati ya watano.

Haikuwa na faida yoyote kwa wale ambao sio wagonjwa sana.

Je majaribio ya dawa hiyo yalikuwaje?

Matokeo ya dawa ya dexamethasone yalifanywa na Chuo Kikuu cha Oxford.

Dawa hii pia inafanya majaribio ya dawa zingine zinazotumika kwa hali tofauti ikiwa zinaweza kutumika kama tiba ya corona.

Takriban wagonjwa 2,100 wanapokea dozi, ya 6mg yaa dawa ya dexamethasone kwa siku 10.

Hali zao zilikuwa zinafananishwa na majaribio ya wagonjwa 4,300 wanaopokea dawa hiyo bila kuchanganywa na dawa nyengine yoyote.

Wanasayansi wanaimani kwamba dawa ya dexamethasone huenda hatimae ikawa sehemu ya dawa, ambayo kwa pamoja, inaweza kupunguza vifo hata zaidi.

Kwa sasa hivi dawa hiyo imependekezwa kwa watu wazima, bila kujumuisha wale wanawake wajawazito au wanaonyonyesha.

Upatikanaji wake uko vipi?

Bei ya dawa ya dexamethasone ni ya chini na tayari inapatikana kwa wingi.

Serikali ya Uingereza imesema kuwa tayari imenunua dawa hizo za kutosha kutibu wagonjwa 200,000, kwa matarajio ya kuwa na matokeo mazuri kutokana na majaribio yanayoendelea.

Uingereza, dawa hiyo itagharimu pauni 5.40 kwa siku kwa mgonjwa mmoja na tiba yenyewe inadumu kwa siku 10.

Mara ya kwanza kutengenzwa ilikuwa ni mwaka 1957 na kuanza kupatikana mapema miaka ya 1960.

Na kwasababu imekuwepo kwa miaka mingi, dawa hii inaweza kupatikana katika maduka ya kuuza dawa na sio lazima kwenda hospitali.

Hili lina maanisha kampuni nyingi zinaweza kuitengeneza na pia inapatikana kote duniani.

Habari ya dawa hii kuwa mwokozi imepokelewa vipi?

Shirika la Afya Duniani (WHO) limefurahishwa na matokeo ya majaribio ya dawa hiyo, na kusema kuwa kwa sasa hivi utafiti mkubwa bado unahitajika kufanywa kwa wagonjwa wenye dalili za wastani - ambao hawawezi kuponywa na dawa hiyo.

Matokeo hayo ni mazuri hasa kwa nchi zinazoendelea.

Mataifa mengi ya Afrika, kwa mfano, gharama ya dawa hiyo ni chini ya dola mbili.

Afrika Kusini, ambako dawa hiyo inatengenezwa, serikali tayari imeshauriwa kuitumia kwa wagonjwa wa corona wanaotumia oksijeni au mashine ya kupumua.

Data kutoka WHO inaonesha kwamba zaidi ya watu 5,000 wamekufa kwa ugonjwa wa Covid-19 Afrika,wengi wao wakiwa ni wale wenye maradhi mengine tayari.

Je inatumika kwa ugonjwa gani tena?

Dawa hii inaweza kutumiwa kutibu magonjwa kadhaa kama vile kuvimba au kufura kwa mwili, au katika hali ambapo mfumo wa mwili umebadilika vibaya wakati wa kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 - , kwa mfano, kwa wanaoshikwa vikali na pumu ambako kunaweza kusababisha kufura katika mfumo wa kupumua na mapafu, athari mbaya ya mzio au maumivu kwenye viungo vya mwili vilivyovimba.

Dexamethasone pia inaweza kutumika pale mfumo wa kinga unaposhambulia chembe nzuri katika hali za ugonjwa kama ule wa yabisi kavu, mabaka mekundu kwenye ngozi ambayo husababishwa na mfumo wa kinga kuvamia au kuanza kushambulia mwili.

Je athari za dawa hii ni zipi?

Athari za dawa hii inapotumiwa kwa magonjwa mengine ni pamoja na kuwa na wasiwasi, kukosa usingizi usiku, kuongezeka kwa uzito na kuzuia majimaji mwilini.

Athari mbaya zaidi ni pamoja na matatizo ya macho, kuathirika kwa uwezo wa kuona na kuvuja kwa damu.

Hata hivyo, wagonjwa wa virusi vya corona wanahitaji dozi kidogo au kiwango kidogo tu cha dawa hiyo ambacho kitazuia athari.