Uchaguzi Tanzania 2020: Fahamu sababu ya Zanzibar kufanya uchaguzi wa mara mbili

zanzibar

Kisiwa cha Zanzibar nchini Tanzania kitashiriki kwenye uchaguzi mkuu mara mbili, ifikiapo Jumanne tarehe 27 mwezi Oktoba na Oktoba 28.

Uchaguzi huo ambao utakuwa wa kihistoria utafanyika kwa siku mbili ili kutoa fursa kwa makundi yaliokuwa yakipata changamoto za kupiga kura kushiriki katika uchaguzi huo.

Akizungumza na mwandishi wa BBC, Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi kisiwani Zanzibar ZEC, Thabit Idarous amesema kwamba lengo kuu ni kutoa fursa kwa makundi tofauti kushiriki katika zoezi hilo.

''Ipo haja ya kufanya mabadiliko ili kuliangazia kundi mahsusi ambalo linakosa haki ya kupiga kura''.

''Watunga wa sheria bila shaka huenda waliona changamoto kutokana na ripoti mbalimbali zilizowasilishwa baada ya uchaguzi ulizopita'', aliongeza.

Kura hii ya awali kwa watumishi wenye majukumu maaalumu wakati wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria, imekuwa ikileta sintofahamu.

Moja ya mataifa ambayo yamekuwa yakifanya uchaguzi wa mapema ni Marekani

Mkurugenzi huyo amewataka wapiga kura kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika zoezi hilo la kihistoria.

'Nawaomba wapiga kura kujitokeza kwa wingi na baada ya kupiga kura waondoke katika vituo hivyo vya kupigia kura na kwenda nyumbani'

Amesema kwamba baada ya kura kuhesabiwa na kuthibitishwa ndani ya siku tatu tume hiyo itatangaza mshindi .

Ameongezea kwamba ni tume ya uchaguzi ya ZEC pekee ilio na haki za kutangaza matokeo hayo.

Wapiga kura laki tano na 66, katika majimbo 50 ya visiwa vya Zanzibar, wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu.

Wakati huohuo Tume ya uchaguzi nchini Tanzania imakana madai kwamba uvumi kwamba kumekuwa na vituo hewa na wapigakura hewa nchini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa tume hiyo amesema kwamba anawahakikishia wananchi kwamba jambo hilo ni la uvumi linalolenga kuchafua tue ya taifa ya uchaguzi ili kuchagua mchakato mzima wa uchaguzi.

Vilievile mwenyekiti wa baraza la vyama vya kisiasa nchini Tanzania John Shibuda naye alifanya mkutano na waandishi wa habari mwisho wa juma lililopita ambapo alitaka kuwaandaa kisaikolojia wagombea mbalimbali wa vyama vya kisiasa kukubali matokeo yatakayotangazwa na tume ya uchaguzi.

''Kila mgombea nakushauri wawe kisaikolojia na fikra tulivu za utarayi wa kupokea matokeo ya kushinda ama kushindwa wa nafasi zinazoshindaniwa kwa viti vya udiwani, ubunge na kiti cha urais na raisi wa Tanzania visiwani mwaka 2020'', alisema.